Jumatano, 19 Juni 2013

CHEGGE ‘aichanachana’ BAJETI YA SERIKALI 2013/14

Kamati ya Bunge ya Bajeti inasema wizara zinatumia zaidi fedha ambazo zimeidhinishwa na Bunge.Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, amesema mwelekeo wa matumizi ya Serikali hauridhishi na kuainishisha changamoto mbalimbali, ikiwamo ongezeko la safari za viongozi na watendaji wa Serikali. Chenge alisema safari za nje zimeongezeka kwa asilimia 12, wakati zile za ndani zina ongezeko la asilimia 18. Alibainisha hayo alipowasilisha taarifa ya kamati yake kuhusu hali ya uchumi kwa mwaka 2012 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2013/14, tathmini ya utekelezaji Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya Serikali. “Mwelekeo wa matumizi ya Serikali hauridhishi. Lipo tatizo katika matumizi ya mafuta na vilainishi serikalini. Tathmini inaonyesha Serikali inatarajia kutumia fedha nyingi zaidi,” alisema Chenge na kuongeza: “Kununua mafuta katika mwaka ujao, ikilinganishwa na mwaka huu wa fedha. Ongezeko hilo linafikia asilimia 19.” Kwa mujibu wa Chenge, bajeti ya Serikali mwaka hadi mwaka zimekuwa zikitumika kwa kiasi kikubwa kulipa madeni, badala ya kutekeleza mipango iliyopangwa mwaka husika. Alisema matokeo yake, miradi haikamiliki kwa wakati na kuiongezea gharama Serikali, alitaka kufanya jitihada za makusudi kudhibiti hali hiyo. Alifafanua kuwa kuna tatizo kubwa la malimbikizo la madeni kwa wizara na idara za Serikali, huku asilimia 70 ya bajeti inayopitishwa ikitumika kulipia madeni. Chenge alisema kamati yake imebaini kuwapo kwa baadhi ya wizara, zinazotumia fedha nyingi zaidi ya zinazoidhinishwa na Bunge. Alisema Julai 2012 hadi Aprili 2013, Serikali ilikopa Sh1.364.7 bilioni kutoka soko la ndani la mitaji.

Hakuna maoni: