Jumatatu, 24 Juni 2013

Nchemba, Msigwa nusura wazichape Dodoma

iv dir="ltr" style="text-align: left;" trbidi="on">
Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu

Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akizozana na wabunge wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa(kulia)mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (wa pili kulia) na Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (wa pili kushoto) baada ya kukutana nje ya ukumbi wa mikutano wa St Gasper,Dodoma jana wakati wa semina ya wabunge ya kuhusu Ukimwi. Picha na Fidelis Felix

Dodoma. Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba jana nusura wachapane makonde baada ya kutupiana maneno ya kashfa, wakituhumiana kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea Jumamosi iliyopita mkoani Arusha. Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu. Wabunge hao wa Chadema hawakuhudhuria kikao chochote cha Bunge kutokana na kwenda mkoani Arusha kwa shughuli mbalimbali, kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wao wa kuhitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika viwanja vya Soweto, Juni 16 jijini humo. Malumbano hayo yanatokana na Nchemba kuituhumu Chadema kuhusika na mlipuko huo, Juni 20 mwaka huu wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema chama hicho kilipanga kulipua bomu hilo ili kuwafanya Watanzania waamini kuwa Serikali ya CCM ndiyo inayohusika na tukio hilo. Ilivyotokea Wakati Msigwa akiingia katika ukumbi huo akiwa ameongozana na Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, walikutana uso kwa uso na Nchemba ambaye alikuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Amour Arfi. Baada ya Nchemba kumwona Msigwa alimkaribisha mchungaji huyo akisema; “Karibu sana bwana, salama lakini?” Hata hivyo, badala ya kujibu salamu hiyo ya Nchemba, Msigwa alikuja juu na kumtuhumu Nchemba kwamba anatoa kauli zinazoweza kuvuruga amani ya nchi. “Wewe ni mtu hatari sana, haya yote yanasababishwa na wewe, mnatumia damu za watu kutafuta madaraka,” alisema Msigwa akimtupia maneno Mwigulu. Baada ya kauli hiyo Nchemba alihoji akisema: “Ki-vipi? Hayo mambo tuyaache, Msigwa achana na haya mambo!” Baada ya Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM kujibu, Msigwa alimsogelea karibu na kumnyooshea kidole, huku akiendelea kumtuhumu kuwa ana siasa chafu zinazopandikiza chuki kwa jamii. Malumbano hayo pia yaliingiliwa na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere ambaye alimuunga mkono Msigwa, huku akimtuhumu Nchemba kuwa ni mtu mbaya katika siasa za Tanzania. Katika kile kilichoonekana kutaka kuweka mambo sawa, Wenje alimvuta Msigwa na kumpeleka ukumbini ili kuepusha shari baada ya wabunge hao kuzidi kurushiana maneno.

Vigogo 200 wahojiwa mabilioni ya Uswisi


Ni kuhusu mabilioni ya fedha yaliyohifadhiwa na Watanzania katika mabenki mbalimbali nchini Uswisi

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema. 

Dar es Salaam. Suala la baadhi ya Watanzania kuhifadhi mabilioni ya fedha nchini Uswisi limechukua sura mpya, baada ya tume maalumu kuwahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara. Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa tume hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema tayari imeshafanya kazi hiyo kwa miezi miwili sasa. Tume hiyo maalumu iliyoundwa na Serikali kwa Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana, inatarajiwa kukamilisha uchunguzi huo wakati wowote kuanzia sasa na kuwasilisha ripoti hiyo katika kikao kijacho cha Bunge. Jaji Werema alipoulizwa na Mwananchi Jumpili maendeleo ya uchunguzi huo, alisema kuwa kazi hiyo bado inaendelea. “Uchunguzi huo unaendelea,” alisema Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa. “Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.” Mwanasheria huyo wa Serikali alikataa kutaja baadhi ya majina ya watu ambao tume yake imewahoji mpaka sasa. Alisema anashangazwa na swali la namna hiyo, kwa maelezo kwamba ni jambo ambalo liko wazi kuwa ni kinyume na maadili kuwataja watuhumiwa wakati huu uchunguzi ukiwa bado unaendelea. Uchunguzi huo unafanyika baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa mwezi Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo. Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni. Jarida la kimataifa la uchunguzi la The Indian Ocean Newsletter toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini. Werema anaripotiwa akiri kuwa uchunguzi huo umefikia ‘hatua ya kutia matumaini’ na wanaendelea na kazi hiyo kwa uangalifu ili kuwa na uhakika wa taarifa wanazozitafuta. Alisema kwamba taarifa ya awali inatarajiwa kutolewa hivi karibuni na tayari idadi kubwa ya wahusika wakiwamo wabunge wameshahojiwa.

Jumamosi, 22 Juni 2013

Lipumba adai bajeti imejaa usiri


Ataka iweke wazi uchambuzi yakinifu, ni wapi fedha za miradi ya maendeleo zitatoka. Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2013/14, inategemea misaada kutoka nje na kwamba haionyeshi wazi upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo. Pia, amesema bajeti hiyo inaonyesha kuwa deni la Taifa linakuwa kwa kasi na kufikia asilimia 50 kitu ambacho ni hatari kwa uchumi wa taifa. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akichambua baadhi ya mambo yaliyomo kwenye bajeti hiyo, Profesa Lipumba ambaye pia kitaaluma ni mchumi alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 imejaa kasoro lukuki. Alisema tatizo lililosababisha kujitokeza upungufu kwenye bajeti hiyo ni Serikali kuanza kujadili matumizi bila kujua mapato yaliyopo ni kiasi gani. “Bajeti yetu imejaa matatizo mengi, kwanza haionyeshi wazi upembuzi yakinifu kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo ni la ajabu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza: “Ni jambo la kushangaza kuona bajeti ya maendeleo ambayo ndiyo muhimu kwa uchumi wa nchi inategemea mikopo ya nje, misaada ya nje na mikopo ya ndani jambo ambalo linazidi kuliongeza Taifa mzigo wa madeni.” Profesa Lipumba,alifafanua kuwa utaratibu mzuri ambao nchi nyingi za Afrika zinatumia katika kuwasilisha bajeti za nchi zao ni kujua kwanza mapato ya nchi ndipo wapange matumizi ya Serikali tofauti na sisi tunavyofanya. Profesa Lipumba alitoa mfano kuwa mara nyingi wamekuwa wakiomba kujua upembuzi yakinifu kwenye mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, lakini jambo hilo limekuwa gumu na limejaa usiri mkubwa. Ajira Akizungumzia suala la ajira alisema, Serikali imekuwa na kigugumizi kueleza wazi mwaka huu wa fedha imeajiri watu wangapi. Alisema “Bajeti ya mwaka jana ilieleza wazi imetoa ajira 7000, lakini mwaka huu wa Serikali imekuwa ikizunguka bila kueleza wazi itatoa ajira kiasi hagi jambo ambalo ni la kushangaza.”

Mbowe, Lema wahojiwa polisi,watoa msimamo


“Chadema tuko tayari kukabidhi ushahidi huu kwa tume huru ya uchunguzi ya Mahakama. Rais Kikwete atumie mamlaka yake ya kikatiba kuunda tume kuchunguza tukio la bomu Arusha ili ukweli ujulikane. Polisi ni watuhumiwa katika jambo hili, hivyo hawana dhamira safi na ushahidi wetu,” Arusha. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema jana, walijisalimisha Makao Makuu ya Polisi ya Mkoa wa Arusha na kuhojiwa kwa zaidi ya saa nne kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini wenyewe huku wakitakiwa kurejea kituoni hapo, Julai 22, mwaka huu. Pia Mbowe na Lema wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi wa kimahakama ili kuchunguza vurugu za Arusha zilizoanza Jumamosi iliyopita baada ya bomu kurushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo pamoja na zile zilizofuatia wakati polisi ilipowasambaratisha wafuasi wa chama hicho kwa mabomu walipokusanyika kwenye Viwanja vya Soweto kwa lengo la kutoa heshima za mwisho kwa marehemu. Wakiongozwa na mawakili watatu, Mbowe na Lema waliwasili polisi saa 3.50 asubuhi na kuhojiwa hadi saa 9.10. Viongozi hao walipokewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Diwani Nyanda kabla ya kutenganishwa kwenye vyumba viwili tofauti kwa mahojiano. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbowe, Lema na wakili Albert Msando walitaja mambo mawili ambayo polisi waliwahoji kwanza ikiwa ni ushiriki wao katika mkusanyiko usio halali kwenye Viwanja vya Soweto, Jumanne iliyopita ambao ulisambaratishwa na polisi. Jambo jingine ambalo polisi iliwahoji ni kauli yao ya kuwa na ushahidi unaohusisha polisi na tukio la bomu lililorushwa kwenye mkutano wa Chadema na kusababisha vifo vya watu wanne huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa. Mbowe alisema kwa pamoja wamewaeleza polisi kuwa hawaamini kama mkusanyiko wa Jumanne iliyopita haukuwa halali kwa sababu waliruhusiwa kuzungumza na wananchi waliokusanyika ili kuwashawishi watawanyike. “Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) wa Arusha, Gilles Mroto ndiye aliyeturuhusu kuzungumza na wananchi wale kuwataka watawanyike na ndicho tulichofanya, lakini tukashangaa kuanza kupigwa mabomu mara baada ya kuwataka watu wanaotaka kutoa heshima za mwisho kwa marehemu kwenda Hospitali ya Mount Meru,” alisema Mbowe. Alisema Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja kuwa naye aliyewaomba viongozi wa Chadema kuwatawanya wafuasi wa chama hicho baada ya kuzuiwa kutoa heshima za mwisho katika viwanja hivyo vinavyomilikiwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Msimamo wa Mbowe Kuhusu ushahidi anaodai unawahusisha polisi na tukio la bomu, Mbowe alisisitiza kuwa Chadema kina ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo lakini alisema hakitaukabidhi mikononi mwa polisi. Alisema hakitafanya hivyo kwa kuwa jeshi hilo ni watuhumiwa wakuu hivyo hawawezi kuwa na dhamira na nia njema katika upelelezi wao. Alisema ndiyo maana badala polisi kuwaona ni msaada, kimeanza kutoa vitisho kwa wote wanaosema waliwashuhudia askari wakishambulia watu kwa risasi kabla ya kuondoka na aliyerusha bomu kwenye gari lao.

Mizengo Pinda: Nasema wapigwe tu

Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Dodoma/Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani. Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola. Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?” Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria. “Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.” Pinda alisema Serikali imedhamiria kurejesha amani nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali ifanye kazi hiyo. Alisema Serikali ina orodha ya watu wanaosemekana kuwa ni vyanzo vya vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara na kushangaa wale wanaopinga kukamatwa kwao. “Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema. Hata hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo awali umetoa kauli nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote, ambao watakaokuwa wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu Katika Ibara ya 13 na Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano. “Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa hilo. “Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni marufuku kwa mtu yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza kumdhalilisha. Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja Katiba?” Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati ya mtu aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria... “Mimi ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.” Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta. Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia katika na kumweleza mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na haja ya kuendelea na hoja hiyo.

Jumatano, 19 Juni 2013

Historia ya kiburudani kuandikwa leo!


Mei 29 baada ya kifo cha marehemu Albert Mangwea, Mwana FA aliandika twitter “Sina uhakika, lakini nimeahirisha shoo yangu mpaka June 14 kama kaka tutakuwa tumeshampumzisha,” alitweet FA.Siku iliyosubiriwa kwa hamu na wadau wa muziki nchini ya tamasha la miaka 13 katika muziki ya Judith Wambura maarufu kama Lady Jaydee na The Finest ya mwanamuziki Khamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ imetimia leo. The Finest ya Mwana FA itafanyika pale Makumbusho jirani na chuo cha IFM, huku miaka 13 katika muziki ya Jaydee inatarajiwa kufanyika Nyumbani Lounge. Baada ya kuahirishwa Mei 31 shoo hizi mbili zote kwa pamoja zinatarajiwa kufanyika leo Juni 14 katika maeneo mawili tofauti hali inayoendelea kuwachanganya mashabiki wengi nani alitangulia kutangaza tarehe awali. Mei 29 baada ya kifo cha marehemu Albert Mangwea, Mwana FA aliandika twitter “Sina uhakika, lakini nimeahirisha shoo yangu mpaka June 14 kama kaka tutakuwa tumeshampumzisha,” alitweet FA. Lakini Jaydee aliahirisha na kusema atatangaza ni lini shoo yake itafanyika, baadaye alikuja kuandika twitter “Ni wiki ndefu kwangu Juni 13 mahakamani, Juni 14 Miaka 13 ya Jide. Juni 15 ni siku yangu ya kuzaliwa, ni Juni ni mwezi wangu,” alitweet Jide. Mwanamuziki FA amesema asilimia 15 ya mapato kutoka katika shoo hiyo, yatapelekwa kwa mama mzazi wa Ngwea. “Nimesema nitoe hela mfukoni kwangu moja kwa moja, niipeleke huku, kwa hiyo chochote nitakacho kipata, nataka kutoa asilimia 15 nimpelekee bi mkubwa,” alisema Mwana FA.

Bei ya bia, sigara zazidi kupanda


Pia bia nyingine zote zimepanda kutoka Sh525 kwa lita hadi Sh578, sawa na ongezeko la Sh51 kwa lita. Kuhusu ushuru magari, umeongezwa kwenye magari yasiyozalisha na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka hadi asilimia 25.Dar es Salaam. Serikali imeendelea kuongeza kodi kwenye magari makuukuu, bia, vinywaji vikali, na baridi kama ambavyo kodi imekuwa ikifanya kila mwaka na kuwaathiri watumiaji. Kutokana na hali hiyo wanywaji pombe na sigara pamoja na waagizaji magari watalazimika kutumia fedha nyingi zaidi ili kupata huduma hizo. Vilevile baadhi ya bidhaa zisizokuwa za mafuta nazo zimefanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi, ikiwamo mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na sigara. Vinywaji hivyo vimeongezwa kodi kwa asilimia 10. Kutokana na bajeti ya mwaka 2013/14 iliyosomwa jana bungeni na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, vinywaji vikali vimepanda kutoka Sh2,392 hadi Sh2,631 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh239 kwa lita moja. Bia inayotengenezwa kwa nafaka nchini ambayo haijaoteshwa imeongezwa kodi kutoka Sh310 kwa lita hadi Sh341, sawa na ongezeko la Sh31 kwa lita. Pia bia nyingine zote zimepanda kutoka Sh525 kwa lita hadi Sh578, sawa na ongezeko la Sh51 kwa lita. Kuhusu ushuru magari, umeongezwa kwenye magari yasiyozalisha na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka hadi asilimia 25. Dk Mgimwa alisema hatua hiyo imelenga kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara, huku ikiongeza mapato kwa Sh510 bilioni.